SAFARI za watu kwenda kupata tiba kwa mchungaji mstaafu Ambilikile Mwasapile wa Kijiji cha Samunge, Loliondo zimeingia dosari baada ya kuanza kunyesha mvua za masika zilizoligeuza eneo hilo kuwa kisiwa.
Mvua hizo zilizonyesha kwa takriban siku tatu sasa zimewafanya watu kushindwa kuingia na kutoka katika eneo hilo, jambo linalosababisha usumbufu mkubwa.
Eneo hilo ambalo lipo bondeni chini ya viunga vya milima Sonjo na mingine limekuwa tumbo la kupokea maji ya mvua na mito inayotiririsha maji yake kuelekea katika kijiji hicho.
Awali kabla ya kuanza kwa mvua hizo, mchungaji Ambilikile Mwasapile anayedaiwa kutoa dawa ya kutibu magonjwa sugu yakiwemo ukimwi na kisukari kwa kutumia dawa za miti shamba aliiomba serikali iboreshe mazingira ya eneo analotolea tiba na njia zinazotumika kukifikia Kijiji cha Samunge.
Kutokana na mvua hizo, serikali ya Wilaya ya Ngorongoro imewataka watu wanaohitaji huduma ya ‘Babu wa Loliondo’ kuvuta subira hadi mvua itakapokoma.
Ombi hilo la serikali limetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Elias Wawa Lali, ambaye alisema mazingira ya hivi sasa katika Kijiji cha Samunge si ya kuridhisha kwa binadamu.
“Mvua ni nyingi mno, kijiji hiki kimekuwa kisiwa, mustakabali wa maisha ya binadamu yako shakani, ninawaomba wale wote wenye nia ya kwenda kwa ‘Babu’, kusitisha kwa muda mpaka mambo yatakapokuwa shwari,” alisema.
Aliongeza kuwa mvua hizo zimeleta tafrani kubwa kwa sababu wale waliopata tiba wanataka kutoka eneo husika huku wale wasiopata kikombe wakitaka tiba hiyo, licha ya mazingira ya kuingia eneo la tukio kuwa magumu.
“Hakika hali ni ya tafrani, kwani mito yote inatiririsha maji eneo la tiba, walio ndani hawawezi kutoka na walio nje hawaingii, panahitajika helikopta kuwanusuru,” alisema.
Katika hatua nyingine, Mchungaji mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Ambilikile Mwasapile, ametishia kusitisha huduma yake hiyo kwa wagonjwa wanaotoroshwa kutoka hospitalini na kupelekwa kwake.
Alisema kuwa kumejengeka tabia kwa baadhi ya watu kuwatorosha wagonjwa katika hospitali wakiwa na dripu za maji, damu huku hali zao zikiwa mahututi.
Alibainisha kuwa tabia hiyo ndiyo inayochangia vifo kwa wagonjwa hao mara wafikishwapo kwake, hivyo kuanzia sasa ameamua kupiga marufuku utoroshaji huo.
“Kuanzia sasa sitawapatia matatibu wagonjwa wanaotoroshwa hospitalini huku hali zao zikiwa mbaya, nafanya hivi kwa sababu tabia hii imeanza kuota mizizi na ndiyo inayochangia vifo kuongezeka,” alisema.
Alibainisha kuwa utoroshaji wa wagonjwa hao ni kitendo cha kinyama na hatari kwani miundombinu ya kufika katika kijiji anachoishi si imara kama inavyofikiriwa.
Alisema watu wanapopeleka wagonjwa wao kwake ni lazima wazingatie miundo mbinu ya kufika kijijini hapo na zaidi barabara ambayo ni mbaya kupitika.
Mchungaji Mwasapile amejizolea umaarufu ndani na nje ya nchi kwa kutoa huduma ya kutibu magonjwa sugu kwa kutumia mti shamba, ambapo kila mwenye kuhitaji huduma hiyo hutakiwa kulipa kiasi cha sh 500 kwa kikombe kimoja cha maji kilichochanganywa dawa inayotokana na mti huo.
Idadi ya magari na watu imekuwa ikiongezeka kadiri siku zinavyosonga mbele, ambapo hivi sasa mgonjwa anaweza kupata dawa hiyo katika kipindi cha siku tatu badala ya siku moja kama ilivyokuwa awali.
0 comments:
Post a Comment