Sunday, March 27, 2011

Serikali kutoa tamko la tiba ya Loliondo leo


Mchungaji Mstaafu, Ambilikile Mwasapile
Neville Meena, Arusha
SERIKALI leo itatoa uamuzi wa kuendelea ama kusitisha tiba inayotolewa na Mchungaji Mstaafu, Ambilikile Mwasapile katika Kijiji cha Samunge, Loliondo, mkoani Arusha. Taarifa hiyo inatolewa huku kukiwa na wasiwasi kwamba huenda tiba hiyo inayotolewa na Mchungaji huyo Mstaafu wa KKKT, ikasitishwa kwa muda kutokana na sababu mbalimbali za kiusalama na kiafya.Habari kutoka Loliondo zinasema kuwa hali ya usafiri ni mbaya na kwamba, hadi juzi jioni msururu wa magari yanayokwenda Samunge ulikuwa mrefu kwa umbali unaokadiriwa kufikia kilometa 20, huku baadhi ya wagonjwa wakiwa na hali mbaya.

 Kadhalika hali ya barabara ni mbaya kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha, huku kukiwa na taarifa za kutokea kwa magonjwa ya mlipuko yanayohatarisha afya za wanaokwenda kupata tiba hiyo ya magojwa sugu.
 Hata hivyo, habari za uhakika ambazo Mwananchi imezipata mjini Arusha zinasema hakutakuwa na amri ya kuzuia tiba hiyo, badala yake hatua madhubuti zitachukuliwa ili kuwawezesha watu wanaokwenda Samunge kukaa muda mfupi na kuondoka tofauti na ilivyo sasa.

Chanzo chetu cha habari kililiambia Mwananchi mjini Arusha kwamba, msimamo wa Serikali wa kutozuiwa kwa tiba hiyo umefikiwa katika vikao kadhaa ambavyo viliongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, vikiwahusisha wakuu wa mikoa jirani na Arusha, wakuu wa wilaya kadhaa, maofisa usalama na polisi.

“Taarifa ya Serikali haiwezi kamwe kupiga marufuku tiba hiyo, ila kubwa ni kuhakikisha kwamba tabu wanazopata watu wanaokwenda huko (Loliondo) zinapungua au kumalizika kabisa,” kilisema chanzo hicho na kuongeza:
 “Ujue watu hivi sasa wameanza kukaa porini kwa muda mrefu wakisubiri kupata tiba na wanakosa huduma muhimu kama chakula na mambo mengine…Sasa serikali imekuwa na 'sympathy' (huruma) na watu hawa, hali haiwezi kuendelea hivi”.

 Habari zaidi zinasema miongoni mwa hatua za awali zitakazochukuliwa ni kuzuiwa kwa magari yote na hasa malori ambayo yamekuwa yakipeleka watu wanaokwenda kupata tiba Loliondo kama hatua ya kudhibiti ajali za barabarani ambazo tayari zimekatisha maisha ya watu kadhaa.

Kauli za Viongozi
Waziri Lukuvi ambaye amekuwa mjini Arusha kwa siku kadhaa kuratibu hali hiyo, aliliambia Mwananchi jana kuwa Serikali itatoa taarifa rasmi leo kuhusu suala hilo .
“Subirini kesho (leo) asubuhi Serikali itatoa taarifa rasmi kuhusu suala hilo. Hawa maofisa wako hapa wanajipinda kuiandaa na kesho saa moja asubuhi watatoa taarifa, tena ya maandishi,” alisema Lukuvi alipozungumza na Mwananchi kwa simu.

Alipoulizwa kuhusu kamati ya wakuu wa mikoa wanaodaiwa kwenda Loliondo juzi kujadiliana na Mchungaji Mwasapile, Lukuvi alikanusha kuwepo kwa kamati hiyo.
 “Kamati gani tena, si kweli kwamba kuna kamati iliyokwenda huko, nyie subirini tu taarifa mtapata na mtawajulisha wananchi,” alisisitiza Waziri huyo ambaye ni miongoni mwa viongozi waliokunywa dawa hiyo yapata wiki mbili zilizopita.

 Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Isdori Shirima, naye alithibitisha kuwa taarifa ya Serikali kuhusu hatima ya tiba ya Loliondo itatolewa rasmi leo bila kutaja muda itapotolewa.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Thobias Andengenye, alisema jeshi hilo haliwezi kutoa kauli yoyote kuhusu suala hilo .

 “Mimi nadhani msubiri yule aliyesema atatoa taarifa rasmi, awape taarifa hiyo… Subirini tu maana si muda mrefu mtapewa,” alisema Andengenye alipozungumza kwa simu na Mwananchi.
 Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Elias Wawa Lali, aliliambia gazeti hili kuwa hana taarifa yoyote kuhusu hali ilivyo sasa Loliondo kwani yupo mjini Arusha ambako alishirikiana na wenzake kuweka sawa taratibu za usimamizi wa wanaokwenda wilayani kwake.
“Mimi sipo huko, niko Arusha labda nitafute baada ya saa mbili hivi naweza kuwa na taarifa zozote kuhusu hali ilivyo hivi sasa.

Wagonjwa warejeshwa
Zaidi ya watu 100 waliokuwa wakisafiri kutoka maeneo ya Uchira na Kiboriloni, mkoani Kilimanjaro kwenda kijiji cha Samunge, Loliondo kunywa dawa ya Babu, wameishia mjini Arusha na kulazimika kurejea nyumbani bila kupata tiba.

 Wananchi hao wengi wakiwa ni wanawake wa makamo, watoto na wazee walilazimika kulala ndani ya lori walilokuwa wakisafiria, likiwa limeegeshwa nje ya Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha, baada ya lori kuzuiwa kuendelea na safari na kisha kukamatwa na polisi.
 Gari hilo aina ya Fusso lilikamatwa juzi majira ya saa kumi jioni katika eneo la Tanapa, nje kidogo ya Mji wa Arusha ambao wanatekeleza agizo la kuzuia magari yasiyokidhi vigezo vya kusafirisha abiria kwenda Kijiji cha Somange.

 Msaidizi wa Mkuu wa Usalama Barabarani Mkoa wa Arusha, Mrakibu Msaidizi wa Polisi Sylivester Ndidi, alisema kuanzia sasa malori na magari yasiyokidhi vigezo vya kusafirisha abiria hayataruhusiwa kwenda Loliondo.
Miongoni mwa watu waliokuwa wakisafiri na lori hilo ni Mzee Peter Ndanu (82), mkazi wa Kirua Vunjo ambaye alikuwa na cheti cha hosipitali kinachothibitisha kwamba yeye ni mgonjwa.

Ndalu aliliambia Mwananchi jana kuwa alilazimika kuchukua cheti hicho kutokana na kuwapo taarifa kwamba polisi wanawazuia baadhi ya watu kwenda kupata tiba hiyo. “Nilikichukua cheti ili kuwathibitishia kwamba mimi ni mgonjwa, ili wasije wakanizuia kwenda kupata tiba..”,alisema Ndalu anayedai kwamba ametibiwa kwa miaka mingi katika hosipitali za hapa nchini jijini Dar es Salaam na mkoani Kilimanjaro bila mafanikio.

Baadhi ya abiria walisema baada ya gari lao kukamatwa lilirejeshwa eneo la  Sheikh Amri Abeid na kuegeshwa hapo na dereva wake, Paul Mkojera, alikamatwa na kuswekwa lupango katika Kituo Kikuu cha Polisi mjini Arusha.
Hali hiyo iliwafanya abiria wa lori hilo kulala ndani ya gari, huku wakisubiri hatma ya safari yao, lakini jana majira ya saa 4.10 asubuhi, ASP Ndindi alifika Sheikh Amri Abeid na kuwaambia kuwa lori hilo haliwezi kuendelea na safari na kwamba watatafutiwa usafiri mwingine wa kwenda Loliondo ama kurejea nyumbani kwao Moshi.

 Ndindi alipofika kuzungumza na abiria hao kuhusu mustakabali wa safari yao, baadhi ya kinamama walimsihi awaruhusu kuendelea na safari hiyo huku mmoja wao akilengwalengwa machozi akimwangukia miguuni.
 Abiria hao walisema usafiri huo walipewa kama msaada kutoka mmoja wa wakazi wa Moshi ambaye hawakumtaja jina na kwamba walitozwa fedha kidogo tu kwa ajili ya kugharamia mafuta.
 “Hapa hakuna mtu aliyetozwa zaidi ya Sh30,000/-, wengine tumetoa Sh15,000, Sh20,000 na nauli ya juu kabisa ni Sh30,000 kwa ajili ya kusaidia kununua mafuta,”alisema msafiri aliyejitambulisha kwa jina la Francis Mswaki, mkazi wa Kirua Chini.

 Mswaki alisema katika eneo ambako gari lao limeegeshwa hakuna usalama kwani baadhi yao tayari walikuwa wameibiwa mali zao. “Mimi tayari nimeibiwa simu, hii ni hasara ambayo sikuitarajia… ..lengo langu na wengine unaotuona hapa ni kwenda kupata tiba kwani tunaumwa, hakuna mtu anayekwenda huko wakati ni mzima,”alisisitiza Mswaki.

 Kauli ya Mswaki kuhusu usalama katika eneo la Sheikh Amri Abeid, inaunga mkono taarifa kwamba kumekuwa na vitendo vya utapeli, udanganyifu, wizi na uporaji wanavyofanywa abiria wanaosubiri kusafiri kwenda Samunge.
 Eneo lililopo nje ya uwanja huo ndilo linalotumiwa na magari yanayowasafirisha abiria wanaokwenda Loliondo na kuna idadi kubwa ya madalali ambao wanalaumiwa kwa kusababisha nauli za kwenda huko kupanda.

Safari za Loliondo sasa zaanzia Dar
Eunice Muhandia anaripoti kuwa kampuni ya usafirishaji abiria ya Chakito ambayo baadhi ya magari yake yanafanya safari za kutoka Dar es Salaam kwenda Arusha, imeanzisha safari ya kutoka Dar es Salaam hadi Loliondo kwa nauli ya Sh130,000.

Mmoja wa mawakala wa kampuni hiyo aliyejulikana kwa jina moja la Said alisema jijini Dar es Salaam jana kuwa kampuni hiyo imefikia hatua hiyo baada ya kubaini ongezeko la abiria wanaokwenda Loliondo kupata tiba kwa Mchungaji Mwasapile.

Wakala wa kampuni ya Happy Nation ambaye hakutaka kutajwa gazetini kwa kile alichoeleza kuwa sio msemaji wa kampuni hiyo, alieleza kuwa nauli za kwenda Arusha sasa zimeanza kushuka. Alisema tofauti na majuma matatu yaliyopita ambopo nauli zilikuwa Sh30,000, sasa nauli zimepungua na kufikia Sh17,000.

Waganga wa tiba asili  waiponda dawa ya Mchungaji
Naye Raymond Kaminyoge anaripoti kuwa, waganga wa tiba asili nchini, wameijia juu Serikali kwa kuruhusu tiba ya Mchungaji Ambilikile Mwasapile wa Kijiji cha Samunge, Loliondo huku ikijua kuwa ni kinyume cha sheria za nchi.
Walisema sheria ya tiba asili namba 23 ya mwaka 2002, inasema kuwa kila mganga wa tiba asili anatakiwa kusajiliwa na dawa zake kupimwa na Mkemia Mkuu wa Serikali kabla hazijaanza kutumiwa.

Katibu Mkuu wa Chama cha Watafiti wa Malaria Sugu, Mazingira na Ukimwi kwa Tiba Asili, (Chawamamu), Abdalaham Mkenga alisema hayo jana jijini Dar es Salaam alipozungumza na Mwananchi kwa simu.
Alisema sheria hiyo imeeleza wazi kwamba yoyote atakayekiuka atafikishwa mahakamani na akipatikana na kosa atafungwa jela miaka miwili au kulipa faini ya Sh 500,000 ama vyote viwili.

“Mbona Babu wa Loliondo hajachukuliwa hatua za kisheria wakati hajasajiliwa wala dawa yake haijapimwa na Mkemia Mkuu wa Serikali kama inafaa kwa matumizi ya binadamu,”alisema Mkenga.


0 comments:

Post a Comment