Friday, April 8, 2011

Mabomu yatawala mjadala wa katiba

VIUNGA vya Bunge mjini Dodoma jana viligeuka uwanja wa mapambano baada ya askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), kutumia mabomu na risasi za moto kutawanya mamia ya wanafunzi wa vyuo vikuu waliotaka kuingia katika ukumbi wa Pius Msekwa kushiriki mjadala wa maoni wa Muswada wa Sheria ya Mapitio ya Katiba.Wakati hali hiyo ikiwa hivyo mjini Dodoma, mkutano wa aina hiyo ulifanyika jijini Dar es Salaam uliovurugika baada ya kutokea vurugu.

Mapambano yaliyotokea mjini Dodoma, kati ya wanafunzi wa vyuo vikuu na FFU yalisababisha wakazi wa maeneo ya Makole, Uhindini, Sabasaba na Mtaa wa Railway kukimbia ovyo huku baadhi yao wakifunga maduka na biashara zao kuhofia kujeruhiwa kwa risasi.Hofu hiyo ilitokana na idadi kubwa ya watu, wengi wakiwa ni wanafunzi wa Vyuo Vikuu vya mjini Dodoma, kulazimisha kuingia kushiriki mjadala huo katika Ukumbi wa Msekwa wenye uwezo wa kuhimili watu 300 ambao tayari ulikuwa umeshajaa.

Katika vurugu hizo, wanafunzi hao walivunja lensi ya kamera ya Mpigapicha wa gazeti hili kwa jiwe walilokuwa wanataka kumpiga nalo Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk James Msekela, wakati akizungumza nao.

Msekela aingilia kati
Vurugu hizo ambazo zililazimisha polisi kupiga  risasi takribani 19 hewani, zilianzaa saa 5:00 asubuhi na kudumu kwa zaidi ya dakika 45. Hata hivyo, wakati risasi zikirindima wabunge na wadau mbalimbali walikuwa wakiendelea na mjadala huo katika ukumbi huo.

Dalili za kuwapo kwa vurugu hizo zilianza kujionyesha mapema kufuatia baadhi ya wanafunzi kuzuiliwa kuingia katika lango la ukumbi huo licha ya kufika mapema.Kuzuiliwa kwa wanafunzi hao kulisababisha baadhi ya wabunge hasa wa Chadema kulazimika kutoka nje ya ukumbi na kwenda kuwatuliza ili wasilete fujo.

“Nawashauri mtumie hekima na busara katika kuingia ndani ya ukumbi huu kwa kuwa ni haki yenu kikatiba, lakini tulieni tufanye utaratibu,”alisema Mbunge wa Kawe, Halima Mdee.Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini, naye alitumia muda mwingi kuwasihi wanafunzi kuacha kutumia nguvu, badala yake watumie hekima.

Mbunge wa Arusha mjini, Godbless Lema, ambaye anabebeshwa zigo hilo la ghasia, naye alitoka ndani ya ukumbi huo wa Msekwa na kuwahutubia wananchi hao waliokuwa wamefunga barabara. Lema anayetajwa kuamsha umma huo kufika viunga hivyo vya Bunge, aliwaambia  wanafaunzi hao  kuwa ni  haki yao kuchangia maoni katika muswada huo kwani unagusa  mustakabali wa nchi na alipinga hatua ya muswada huo kujadiliwa na mikoa mitatu (Dodoma, Dar es Salaam na Zanzibar).

Dk Msekela alimlaumu Lema kwamba ndiye chazo cha wanafunzi kujitokeza kwa wingi.
“Matatizo haya yamesababishwa na Lema ambaye jana alikwenda katika vyuo vikuu kuwahamasisha wanafunzi wafike kujadili muswada huo,” alisema Dk Msekela.Hata hivyo, Lema aliyekuwa amesimama nyuma ya Dk Msekela, alijitokeza na kukiri kufanya hivyo na kusisitiza kwamba hataacha kufanya hivyo kwa kuwa ni haki yake.

“Mimi Lema ndiye niliyekwenda UDOM kuwahamasisha waje kwa kuwa hawa ni wasomi na muswada umeandikwa kwa lugha ya Kiingereza, hivyo wananchi wa kawaida hawawezi kuujadili tusipowaleta wasomi kama hawa," alisema Lema na kusisitiza:
"Sitaacha kwenda vyuoni kwani Jumamosi (kesho) nitakwenda kufungua tawi huko."
Awali wanafunzi walikuwa wakiimba nyimbo mbalimbali za hamasa zikiwamo nyimbo za Taifa pamoja na wimbo maalumu ambao hutumiwa na wanafunzi wa Vyuo vikuu unaosema, "Kama sio juhudi zako Nyerere, mafisadi wangetoka wapi."Wakiwa na mabango yenye ujumbe mbalimbali, wanafunzi hao walisema hawatoki katika eneo hilo na wako tayari kwa lolote.

Barabara zilifungwa
Barabara ya Kati Dodoma ilifungwa na wanafunzi hao na kusababisha magari kutumia njia ya Dodoma Inn (Barabara ya kwanza) ambayo ina mzunguko mrefu.Wananchi katika maeneo ya Makole, Uhindini, Sabasaba na Mtaa wa Railway walitaharuki na kukimbia ovyo huku baadhi yao wakifunga maduka na biashara zao kuhofia mirindimo ya risasi.

Tambwe achafua
hali ya hewa Dar
Wakati Dodoma kukiwaka moto, mjadala huo ulifanyika pia katika Ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam, lakini haukuisha vizuri baada ya Mkuu wa Kitengo cha Propaganda cha CCM, Tambwe Hizza kuchafua hali ya hewa.
Hizza ambaye alikuwa ni msemaji wa 10 na wa mwisho akiwakilisha CCM , alishindwa kuendelea na mada yake baada ya washiriki wa kongamano hilo kupiga makofi ya bila mpangilio huku wakimzomea.

Akitoa hoja yake, Tambwe  alianza kwa kumpongeza Rais Jakaya Kikwete kwa kile alichokiita kuonyesha nia ya kupatikana kwa Katiba mpya na kwamba kupinga muswada huo ni matokeo ya mfumo wa vyama vingi ambao unaruhusu tofauti ya mawazo.

“Tangu nchi yetu iliporuhusu mfumo wa vyama vingi tulijua kutakuwa na mawazo tofauti,” alisema Hizza huku akirushiwa maneno  ya kebehi na washiriki wakisema "Jadili muswada"
Lakini Hizza aliendelea kusema, “Wote tunataka Katiba mpya.  Kwa mujibu wa Ibara ya 98 ya Katiba ya sasa, mabadiliko ya katiba yanaweza kuwa ni kubadilisha, kufuta au kuirekebisha ,kwa hiyo jina tu marejeo ya katiba katika muswada huu lisiwape tabu.”

Washiriki walimzomea Tambwe huku wengine wakipiga makofi, lakini yeye aliendelea kuzungumza bila kujali kelele zao. Wakati washiriki wakiendelea kumzomea Tambwe, Mwenyekiti wa mdahalo huo, Mbunge wa viti Maalumu, Pindi Chana (CCM), aliwataka washiriki wa kongamano hilo kunyamaza na kumsikiliza Tambwe.

Ushauri huo Chana haukuweza kuwatuliza badala yake walizidisha kelele huku wakimzomea wakisema, “Aondoke..., aondoke, aondoke, aondoke…”. Hali hiyo ilidumu kwa dakika tano, kisha Chana alitangaza kuahirisha kongamano hilo na Tambwe akarudi kuketi sehemu yake.

Uamuzi wa Tambwe kuketi ulizidi kuwasha moto kwani washiriki walianza kuzozana na nusura ngumi zipigwe, lakini askari polisi waliokuwapo katika ukumbi huo walifanikiwa kutuliza ghasia.

Vijana wazozana
Hali hiyo ilionyesha wazi kuwapo kwa makundi makubwa mawili ya Chadema na CCM, ambayo yalipingana, huku baadhi ya vijana wa chama tawala wakiwashutumu vijana wenzao wa chama pinzani, wakidai kuwa chama hicho kimewapa fedha ili wakafanye fujo.

“Chadema wamewapa fedha mje kufanya fujo, tuna ushahidi hata kijana wetu mmoja naye amepewa,” alisema Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Kinondoni, Emanuel Makene. Hata hivyo, kauli hiyo ilipingwa na mzee aliyejitambulisha kwa jina la Salim Nyambua Said, akisema CCM wamekosea kuleta watu wasio makini kwenye kongamano hilo,
“Chanzo cha vurugu hizi ni CCM kuleta wahuni.'' Kauli hiyo ilimsababisha kutaka kupigwa na vijana wa chama tawala kabla hajaokolewa na polisi.

Vijana wengi waliokuwapo nje ya ukumbi huo, walisisitiza kuwa hawahusiki na Chadema na kwamba wao hawakuridhishwa na maneno ya Tambwe. “Sisi hatuhusiki na Chadema, ila tumekerwa na Tambwe Hizza, badala ya kujadili muswada anaviponda vyama vya upinzani,” alisema kijana mmoja ambaye hakutaka kutaja jina lake.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuvunjika kwa kongamano hilo, Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa, alisema kuna vijana wameandaliwa kufanya vurugu. “Yanayotokea hapa inaonyesha kuna vijana wameandaliwa, au hawakuandaliwa kuja kufanya fujo, mimi nawashauri kuheshimu mawazo ya watu hata kama hawayataki,” alisisitiza Tendwa.

Jaji Warioba
Vurugu katika kongamano hilo zilianza kujionyesha pale aliposimama Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba, ambaye alianza kwa kumsifu Rais Kikwete kwa kuanzisha muswada huo akisema ni hatua nzuri.

“Muswada huu ni hatua ya ya kuelekea kwenye utaratibu wa kupata Katiba mpya…. Nafikiri hii ni hatua kubwa. Tunayo Sheria ya kuunda Tume ambayo Rais angeweza kuitumia, lakini kwa umuhimu wake ameunda tume ambayo atakuwa akipata ushauri, mimi sioni tatizo,” alisema Jaji Warioba na kuonekana kuwakasirisha washiriki wa kongamano hilo walioanza kuguna na kupiga makofi mfululizo na kumfanya ashindwe kuendelea kuzungumza.

Hali hiyo ilimfanya Pindi Chana, kuwatuliza washiriki ili Jaji Warioba aweze kuendelea kuzungumza.
Kwa kusoma upepo, Jaji Warioba akabadilisha mwelekeo na kuanza kuukosoa muswada huo hali iliyowafanya washiriki hao kutulia kimya na kumsikiliza.

Jaji Warioba alikikosoa kifungu cha 9 (2) kinachozuia mambo kadhaa kujadiliwa, aliyaita mambo hayo kuwa ni matakatifu. “Kifungu cha 9 (2) kimeweka mambo matakatifu ambayo hayapaswi kuguswa. Haya ndiyo Katiba yenyewe, tunachotaka watu watoe maoni yao,” alisema.

Kongamano hilo baada ya kufunguliwa na Waziri wa Nchi Katiba Ofisi ya Rais, Utawala Bora, Mathias Chikawe, lilikuwa na wasemaji kutoka vyama vya siasa na taasisi mbalimbali.

Viongozi wa vyama vya siasa walikuwa ni Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilbrod Slaa, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa APT Maendeleo, Peter Kuga Mziray, Mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi, James Mbatia na Katibu wake, Sam Ruhuza.

Pia walikuwapo wawakilishi wa taasisi zisizo za kiserikali kama Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kilichowakilishwa na Imelda Urio.Wengine ni Dk Modesta Opiyo kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe, Gideon Mandes kutoka vyama vya walemavu na Dk Francis Michael. Kwa ujumla, wachangiaji wote waliukosoa muswada huo na kutaka ufanyiwe marekebisho.


0 comments:

Post a Comment