Monday, April 11, 2011

Mkama, Kinana watajwa kubeba jahazi la CCM

SIKU moja baada ya Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kujiuzulu pamoja na sekretarieti yake, baadhi ya makada wa chama hicho tawala wanatajwa kujaza nafasi za utendaji.Taarifa kutoka ndani ya kikao cha Halmashauri Kuu jana usiku mjini hapa zilidai kuwa Wilson Mkama ndiye aliyepewa jukumu la Ukatibu Mkuu wa CCM huku msaidizi wake kwa upande wa Bara akitajwa kuwa ni Abdulrahman Kinana, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, Katibu wa Fedha na Uchumi, Zakia Meghji na Katibu wa Oganaizesheni, Dk Rehema Nchimbi.
Kuhusu Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, inadaiwa kuwa Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete aliwasilisha jina la Saleh Ramadhan Feruzi, lakini lilikataliwa na wajumbe kutoka visiwani.
Sekretarieti iliyojiuzulu ilikuwa inaundwa na Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba, Naibu Makatibu Wakuu bara na visiwani; George Mkuchika na Feruzi, Katibu wa Itikadi na Uenezi, John Chiligati, Katibu wa Fedha na Uchumi, Amos Makala,Katibu wa Oganaizesheni, Kidawa Saleh na Mambo ya Nje, Bernard Membe.
Mkama akishirikiana na Profesa aliyefahamika kwa jina moja la Luhanjo, ndiyo waliofanya tathmini ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana na kupendekeza kwamba lazima baadhi ya wanachama watoswe kuokoa chama hicho.
Inadaiwa kuwa miongoni mwa ajenda za kikao hicho ni kujivua gamba ambayo hatua ya kujiuzulu kwa sekretarieti na kamati kuu ni utekelezaji wake.
Inadaiwa kwamba kujiuzulu kwa Kamati Kuu kulitokana na mvutano wa wajumbe ambao walionyesha kugawanyika, huku kundi moja likitaka Mbunge wa Igunga na Mjumbe wa CC, Rostam Aziz, Mbunge wa Bariadi Mashariki na mjumbe wa kamati hiyo, Andrew Chenge wajiuzulu na jingine likipinga.
Baada ya mvutano mkali wa wajumbe hao na kuchukua muda mrefu, inadaiwa Rais Kikwete aliilazimisha kamati nzima kujiuzulu.Awali, ilidaiwa kuwa ajenda hiyo ya kuwataka wajumbe hao wawili wajiuzulu ingewasilishwa kwenye kikao cha Halmashauri Kuu, huku kundi linalodaiwa kupinga ufisadi likitaka wafukuzwe uanachama.

WanaCCM Dodoma wachekelea
Katika hatua nyingine, kujiuzulu kwa Sekretarieti na Kamati Kuu ya CCM kumeonekana kuwakuna baadhi ya wananchi na wafanyakazi wa chama hicho hasa wale wa Makao Makuu, Dodoma.Baadhi ya wafanyakazi hao na wananchi wakiwa kwenye makundi, walikuwa wakijadili hatua na kupongeza uamuzi huo na kwamba, hivi sasa chama hicho kimeamua.
“Tunaomba waandishi msituzibe tunataka kuwaona viongozi wetu, maana leo siyo sura tulizozoea wamejivua gamba,” walisikika wafanyakazi hao wakati Mwenyekiti wa CCM, Rais Kikwete alipokuwa akiingia kufungua mkutano wa Halmashauri Kuu.Tofauti na kawaida yake ya misemo na uchekeshaji, sura ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba ilionekana ya upole wakati akimkaribisha Rais Kikwete.


0 comments:

Post a Comment