Sunday, April 17, 2011

Slaa ataja mafisadi wapya

WAMO VIGOGO WA CHAMA, WAZIRI MMOJA
   KATIBU Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa na kada wa chama hicho, Mabere Marando, jana walitaja orodha mpya ya waliyodai kuwa ni mafisadi.Akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Chipukizi mjini Tabora, Dk Slaa aliwataja mafisadi hao kwa majina yao (yamehifadhiwa)kuwa ni pamoja na Waziri Mkuu mstaafu mmoja ambaye alimtuhumu kuhusika na wizi wa fedha za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA).

Mwingine ni Rais mmoja mstaafu na waziri mmoja aliyekuwa Serikali ya awamu ya tatu na sasa yuko katika Serikali ya awamu ya nne kwa tuhuma za kuhusika na kuuza nyumba za Serikali bila kufuata utaratibu.

Wengine ambao wametajwa na Dk Slaa ni Katibu Mkuu wa zamani wa CCM ambaye amewahi kushika nyadhifa nyingine serikalini kwa tuhuma za kuhusika na EPA.

Wengine ni wafanyakazi wawili wa kampuni moja inayomilikiwa na kada mkongwe wa CCM ambao wanatuhumiwa kuchota mabilioni ya fedha kupitia Kampuni ya Kagoda ambao walitajwa na Marando.

Akifafanua tuhuma hizo, Marando alisema aliwafuatilia watuhumiwa hao wa kampuni  ya kada huyo wa CCM na kugundua kuwa waliandika majina bandia katika hati za usajili wa Kagoda.

Marando alisema anaishangaa Serikali kutowachukulia hatua watu hao hadi sasa.

Alisema kama Serikali imeshindwa kufanya hivyo yeye ataisaidia kwa kuwa anao ushahidi wote.

"Tulipowataja mafisadi CCM walikanusha, sasa leo wanaibuka na kuwataja mafisadi hao na kuwataka wajiuzulu, huo ni uongo na sidhani kama watajiuzulu kwa kuwa wana urafiki mkubwa," alisema Marando.

Dk Slaa alitaja orodha hiyo katika mkutano huo ambao kabla ya jana ulipangwa kufanyika baada ya maandamano yao yaliyolenga kupinga Muswada wa Marejeo ya Katiba 2011, ambao tayari umeondolewa bungeni.

Dk Slaa alilituhumu Jeshi la Polisi kwa kushindwa kuwachukulia hatua yoyote watuhumiwa hao tangu walipotajwa na chama hicho mwaka 2007 na kuongeza kuwa ataendelea kuwataja kwa kuwa haogopi na yuko tayari kufa.

Alisema kauli inayotolewa na Rais Jakaya Kikwete kwamba nchi iko katika hali tete, inasababishwa na yeye mwenyewe kushindwa kuwachukulia hatua mafisadi.

Miaka minne iliyopita,Septemba 15, 2007 katika viwanja vya Mwembeyanga wilayani, Dk Slaa aliwataja vigogo 11 wanaodaiwa kuwa ni mafisadi.

Awali, msafara wa Dk Slaa ukiongozwa na pikipiki zaidi ya 30 na magari ya polisi uliwasili katika uwanja huo wa mikutano saa 9:47 alasiri, huku ukishangiliwa na mamia ya watu waliofika uwanjani hapo.

Dk Slaa aliongozana na aliyekuwa mgombea ubunge Jimbo la Segerea, Fred Mpendazoe, Profesa Abdallah Safari, Mabere Malando, Wilfred Rwakatale na Mkurugenzi wa Masuala ya Bunge na Halmashauri wa chama hicho, John Mrema.

Katika mkutano huo pamoja na Dk Slaa,wanachama na viongozi mbalimbali walipewa nafasi ya kuzungumza na kwamba Profesa Safari alizungumzia nyumba za serikali zilizouzwa pamoja na udini.

Kwa upande wake, Mpendazoe alizungumzia mwelekeo wa CCM na kifo chake kabla ya Dk Slaa kupigilia msumari wa mwisho kwa kutaja orodha mpya ya mafisadi.

“Wananchi hameni CCM, CCM kwa sasa ninaelekea kufa,”alisema Mpendazoe.

Mpendazoe ambaye awali alikuwa CCM kabla ya kutimkia CCJ na kisha kuhamia Chadema, aliichambua CCM na viongozi wake wapya akisema kuwa ni chama legelege kilichosabisha kuwa na Serikali legelege.

Alisema hata kauli Mwenyekiti wa CCM, Rais Kikwete kuwa chama hicho ‘kimejivua gamba’ ni ya kinafiki kwa kuwa chama hicho imeoza kuanzia kwenye mashina na matawi yake.

Mpendazoe alisema ulegevu wa CCM ulidhihirika katika sakata la kulipa ama kutoilipa Kampuni ya kufua umeme ya Dowans baada ya viongozi wa chama hicho na Serikali kugawanyika, wengine wakitaka Dowans ilipwe na wengine wakipinga.

Alisema kama kweli CCM kimedhamiria kujivua gamba, Katibu Mwenezi wake, Nnape Nauye, anatakiwa kuwataja kwa majina watuhumiwa wa ufisadi ambao CCM imewataka watoke ndani ya chama hicho na siyo maneno tu.

Awali, kundi la wasanii wa Chadema lilitoa burudani za nyimbo mbalimbali zilizogusia mauaji ya mkoani Arusha, uundwaji wa Katiba mpya itakaoushirikisha umma pamoja na ufisadi.

Hata hivyo, jana asubuhi baada ya maandamano ya chama hicho kuahirishwa kufuatia kuondolewa bungeni Muswada wa Marejeo ya ya Katiba 2011, kuliibuka taarifa kuwa mkutano huo usingefanyika hivyo kuwachanganya wananchi, kabla ya kutangaziwa upya kuwa mkutano huo utafanyika kama ilivyopangwa.

CCM na mafisadi

Naye Raymond Kaminyoge anaripoti kutoka Dar kuwa, Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimesema kimegundua mbinu za mafisadi kutaka kumchafua Mwenyekiti wake Rais Kikwete na familia yake kupitia vyombo vya habari.

Vilevile, CCM imerejea kuwataka watuhumiwa wa ufisadi kuondoka kwenye Kamati Kuu ya chama hicho kwa amani, bila kukichafua chama.

Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Bakhresa Manzese jijini Dar es Salaam jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nnauye alisema mafisadi wametangaza vita ya kumchafua Mwenyekiti wa chama hicho na familia yake kupitia vyombo vya habari.

Alisema wamegundua mpango huo na kwamba sasa wanatangaza kuamua kupambana nao hadi wang'oke ndani ya CCM.

"Mafisadi waenguliwe katika Kamati Kuu kwani wametangaza vita ya kumchafua Rais Kikwete na familia yake, sasa tutapambana nao mpaka tuwaondoe," alisema Nnauye.

Aliwataka mafisadi waondoke kwa amani ndani ya chama hicho, na kuwaonya kuwa wasianzishe vita ambavyo hawataviweza.

"Mafisadi wapo kwenye nyumba ya vioo wanaanzisha vita ya mawe wataweza? alihoji Nape."


0 comments:

Post a Comment